Jinsi ya Kuomba

Sala ya Asubuhi

Anza kwa kutamka maneno haya ya imani:

"Nimekubali kununuliwa kwa Damu ya Yesu Kristo. Kuishi kwa roho na kuenenda kwa roho."

Kisha, mwite Roho Mtakatifu kwa msaada wa andiko kutoka Warumi 8:26:

"Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa."

Tamka sala hizi:

1. "Karibu Roho Mtakatifu unisaidie udhaifu wangu katika nafsi yangu, roho yangu, na mwili wangu hapa duniani na Mbinguni katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti."

2. "Karibu Roho Mtakatifu uniombe kwa kuugua kusikoweza kutamkwa kiroho, kinafsi, na kimwili hapa duniani na Mbinguni katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti."

3. "Karibu Roho Mtakatifu unisaidie udhaifu wangu wa asubuhi ya leo, mchana wa leo, jioni ya leo, na usiku wa leo hapa duniani na Mbinguni katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti, Amina."

4. "Karibu Roho Mtakatifu unitetee kwa kuugua kusikoweza kutamkwa asubuhi ya leo, mchana wa leo, jioni ya leo na usiku wa leo hapa duniani na Mbinguni katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti, Amina."

5. "Karibu Roho Mtakatifu unisaidie udhaifu wangu katika huduma yangu, elimu yangu, kazi yangu, miradi yangu, ndoa yangu, biashara yangu, uzao wangu, ukoo wangu, kabila langu, na ardhi yangu hapa duniani na Mbinguni katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti, Amina."

6. "Karibu Roho Mtakatifu uniombe kwa kuugua kusikoweza kutamkwa katika huduma, elimu, biashara, ndoa, uzao, ukoo, kabila, ardhi, miradi, uchumi, na kazi yangu hapa duniani na Mbinguni katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti, Amina."

Baada ya sala hizi:

Kaa kimya kwa muda wa dakika mbili na sikiliza sauti ya Neno lolote ambalo Mungu atakuambia.

Kisha, soma Zaburi 28, Zaburi 51, na Zaburi 91.

Ukimaliza kusoma, unaweza kuimba wimbo wa kuabudu kwa sauti au kimya, kulingana na sehemu ulipo.

Sala ya Mchana

"Ee Mwenyezi Mungu, shughulika na mimi, kinafsi, kiroho na kimwili na ujidhihirishe uwezo wako, ukuu wako, utukufu wako, jina lako, mapenzi yako, ufalme wako, na nguvu zako, kwenye maisha yangu yote, biashara yangu yote, miradi yangu yote, uzao wangu wote, ukoo wangu wote, kabila langu na ardhi yangu yote, katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti."

Soma Mathayo 6:9-13.

Sala ya Jioni

Anza kwa kusifu nyimbo za Kikristo. Kisha, jinunue, jitakase, jifunika, na kujificha kwa Damu ya Yesu Kristo kupitia Mathayo 26:28 na Ufunuo wa Yohana 12:11.

Sali kwa kusoma Zaburi 51, Zaburi 20, Zaburi 35, Zaburi 103, na Isaya 54:14-17.

Ukimaliza kusoma, sema neno hili:

Atukuzwe Mungu aliye juu Mbinguni — Mara 21.

Sala ya Usiku wa Manane 

Anza kwa kusifu, kisha futa kila tamko lililotamkwa la kiganga, kichawi, kijini na kipepo hapa duniani na Mbinguni kupitia kitabu cha Isaya 7:7:

“Bwana MUNGU asema hivi, Neno hili halitasimama wala halitakuwa.”

Baada ya hapo, lamba chumvi kidogo kama ishara ya kuondoa mapooza kwa kusoma 2 Wafalme 2:21:

“Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza.” 

Hili litimie hapa duniani na Mbinguni, kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti.